Tetezi zimezuka kuwa watu watano kati ya saba walioteuliwa kusimamia uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2027 huenda wakawa na uhusiano wa karibu na Rais William Ruto pamoja na Kiongozi wa ODM Raila Odinga – jambo ambalo linaendelea kuzua gumzo na mjadala mkali miongoni mwa Wakenya.
Kiongozi wa chama cha National Liberal Party (NLP), Bw. Muli, amesema kuwa utata huu uliibuka tangu mwanzo wa mchakato wa kuunda jopo la uteuzi wa makamishna wa IEBC. Kwa mujibu wa Bw. Muli, jina lake liliondolewa katika hatua za awali, jambo linaloonesha kuwa mchakato huo haukuwa huru wala wa haki.
Bw. Muli amesisitiza kuwa kwa sasa hakuna kiongozi anayeweza kumlaumu mwenzake kuhusu suala hilo, kwani mchakato mzima ulikuwa na dosari za wazi. Hata hivyo, ametoa wito kwa wananchi kujiandaa kwa uchaguzi wa 2027 kwa kujitokeza kwa wingi na kufanya uamuzi wao wa kikatiba kwa umakini na kwa uhuru.
“Huu ni wakati wa Wakenya kuamua hatima yao. Tuuchukulie uchaguzi huu kama fursa ya kufanya mabadiliko halisi,” alisema Muli.
Kwa sasa, macho yote yameelekezwa kwa tume ya uchaguzi na mipango yake kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027 huku Wakenya wakisubiri kwa hamu hatua zitakazochukuliwa kuhakikisha uwazi na haki katika zoezi hilo muhimu la kidemokrasia.
///